Wednesday, September 7, 2011

Zawadi sehemu ya sita...

''Zawadi, Zawadiiii'' ndio maneno yaliyoniamsha asubuhi ya pili.Nilifumbua macho yangu taratibu na kivivu ili kujua aliyekua ananiamsha ni nani. Mama alikua ameinama akinitazama usoni huku mkono wake mmoja ukiwa umenishika begani.
''Mama, shkamoo.'' nilimsalimu kwa sauti ya chini huku nikifumba macho yangu tena. ''Marahaba mwanangu, unaendeleaje?'' aliuliza bila kuondoa mkono wake begani mwangu. ''Nafuu mama! Umekuja na baba?'' swali hilo lilinitoka kabla sijayafumbua macho yangu na kuyaangaza mle chumbani kuona kama baba alikuwapo.
'' Nimekuja nae ila yupo hapo nje anaongea na sijui ndo mwalimu wako yule.Alafu ilikuaje yeye ndo aliyekuleta hospitali , mashoga zako nao wako wapi?'' japo aliuliza kwa sauti ya utaratibu kama kawaida yake nilihisi shauku ya udadisi ndani yake. Nilifikiria kwa sekunde kadhaa nimjibu nini kisha nikamjulisha kwamba niliwaomba watangulie tulipotoka shule na ningeungana nao baada ya kuongea na mwalimu kuhusu mitihani tuliyokua tukitarajia kuanza jumatatu, na nilipokua naongea na mwalimu ndipo nilipoanguka. ''Ahhhh ndo matatizo ya kutokua na pesa haya. Ungeshatibiwa tangu unaanza kujisikia vibaya haya yote yasingetokea.'' Jibu lake lilionyesha kuridhishwa na langu, ila lilinifanya nijihisi kama mkosaji kwa kumfanya mama ajione kama mzazi asiyeweza kutosheleza mahitaji ya mwanawe, hata pale anapokua mgonjwa. Nilitamani kutoa maneno ya kumfariji ila kabla sijafanya hivyo mlango uligongwa na kufunguliwa mara hiyo hiyo.

Wa kwanza kuingia alikua baba aliyekua amevalia kama ambavyo hua anavaa siku zote akielekea kwenye shughuli zake , kaptula, shati na ndala chakavu kiasi.Bila kusahau kofia yake chakavu aliyotumia kujikinga na jua. Japo kua ilikua imetoboka sehemu kadhaa juu na pembeni bado aliivaa kila siku. Rangi yake ya kijani ilikua imefifia kana kwamba ilikua imedumbukizwa kwenye jiki kwa nia ya kupoteza rangi yake ya awali . Nyuma yake alifuatiwa na mwalimu kisha daktari yule mrembo aliyenihudumia jana yake.
''Hujambo mama?” alinisalimu baba kabla sijatoa shikamoo niliyokua najiandaa kumpa. “Salama tu shikamoo baba!” nilimjibu huku nikimtazama ili niweze kumsoma alikua katika hali gani. Uso wake ulionyesha kuchoka kama ulivyokua wa mama ila alijitahidi kutabasamu hivyo nikajua alikua sawa.
Mwalimu yeye alisimama karibu kabisa na mlango huku akimtazama daktari ambae kwa wakati ule alikua akinipima. “Mrembo naomba uvute hewa ndani kwa sekunde chache kabla ya kuiachia kisha usubiri tena kwa sekunde chache kabla ya kuvuta tena ndani.” maagizo hayo ya daktari yaliambatana na mkono wake mmoja ukisogeza kifaa chake kila kona ya kifua changu upande wa kushoto huku mwingine ukiwa umekishikilia kilipoishia sikioni mwake.
“Mapigo ya moyo yako normal, sasa ngoja niongee na wazee kidogo .Nikirudi nikute bado unapumua ehhhh!!!.” aliniambia mimi uso wake ukiwa umejaa tabasamu lililoonyesha meno yake meupe yaliyojipanga vyema kabla ya kugeuka walipokua wamesimama baba na mama na kuwaomba wamfuate. “Kama hamtojali naomba twendeni ofisini tukaongee kidogo.”


Kuondoka kwao tulitubakisha mimi na mwalimu pekee mle chumbani.Dakika kadhaa zilipita bila ya yeyote kati yetu kusema neno na wala mwalimu hakusogea hata hatua moja kutoka pale alipokua amesimama tangu alipoingia mle ndani. Macho yake aliyaelekeza kwangu ila sidhani kama alikua akiniona maana alionekana mtu mwenye fikira zilizo mbali na pale alipokuwepo. “Mwalimu!!!” nilimwita na kumtoa katika dimbwi la fikira alilokuwamo. “Ehhh niambie mama.” alisema huku akilazimisha tabasamu ambalo lilipingana na matakwa yake. “ Jana ulikua unamuulizia mzee Fadhili sasa umemwona. Alafu mama kaniambia kwamba mlikua mnaongea na baba, mlikua mnaongea nini?” niliuliza kwa shauku. “Ahhh nothing really, stori tu za kawaida kati ya mzazi na mwalimu.Zawadi embu naomba nikuulize kitu.” sentensi yake ya mwisho sikuipenda sana hivyo nikajifanya kama vile sikusikia kipengele hicho , “ Kwahiyo mlikua mnaongelea grades , vitabu, nomino and the likes?” nilimuuliza huku nikiwa nimemtolea macho maana nilipenda sana kujua walichokua wakiongelea na baba.
Enheeee, yani we kama mtabiri vile.Alikua ananiuliza nadhani utafanyaje kwenye mitihani ya mwisho hii alafu kabla sijasahau akaniambia ni kwa kiasi gani anavyokuamini. Anasema japo ni mtoto wa kike bado ana imani na wewe na kwamba Mungu akijalia na wewe ukiendelea ulivyo utafika mbali uukimbie umasikini. Anakuaminia sana ,kama mimi tu.” maneno haya yalinigusa kwasababu sikuwahi kujua baba alinichukulia vipi kama mwanae. Hakua muongeaji sana tulipokua nyumbani na hata nilipompa report card yangu kila mwisho wa muhula hakuwahi hata kuniambia hongera ama najitahidi zaidi ya kuniambia nikazane na elimu maana ndio ufunguo wa maisha, kunipa hongera na kunisifia ilikua kazi ya mama. Mara kadhaa baba aliwahi kuhusisha hali yetu na maisha na kile alichokiita ukosefu wa nafasi ya kuelimika kwenye familia yake. Sikuwahi kuelewa kwanini japo wajomba zangu upande wa mama walikua wanajiweza sana hawakupenda kumsaidia dada yao ili nae maisha yamwie na nafuu kidogo. “Mhhhh owwkeey!! Binafsi hajawahi kuniambia chochote.” nilijibu kwa sauti ya unyonge ambao kwa wakati ule sikujua umetokea wapi. Pamoja na kwamba baba alijitahidi sana kufanya kazi ili hata siku moja nisije nikachelewesha ada sikujua kwamba alijivunia kunipeleka shule. Nilidhani anafanya vile kutimiza wajibu kama mzazi tu na sio vinginevyo. Baada ya kujua kwamba alijivunia kunipeleka shule na kuamini kwamba nilikua naitendea haki nafasi ya kupata elimu kisawasawa nilijikuta nafurahi na kusikitika kwa wakati mmoja. Nilitamani kwamba ningekua nimesikia maneno hayo kutoka kwake mwenyewe hapo kabla.

“Kwahiyo nikuulize?” swali la mwalimu lilinitoa katika mawazo na furaha yangu ya kukubalika kwa baba. “Mhh...owkey uliza tu.” sikuona ubaya hivyo nikampa ruhusa yangu. Ni kama vile alikua akisubiria pia ruhusa ya kusogea karibu na nilipokua maana baada ya kumjibu hivyo alipiga hatua kadhaa kabla ya kufika pembeni ya kitanda nilichokua nimelalia na kuniuliza “Unajua kwamba nakupenda sana?” huku akiwa ananitazama machoni.
“Umewahi kuniambia.” ndilo jibu nililimpa. Sikua na uhakika kwanini aliniuliza na vile na alitaka nimjibu nini hivyo nikachukua kile lililonijia kichwani na kulitoa bila kufikiria mara mbili.
“Najua nimewahi kukwambia, nnachotaka kujua ni kama wewe unajua na kuamini hivyo Zawadi.”
I don't know, labda. Kwani we kwanini unauliza?” nilimjibu na kumtupia swali hapo hapo. “ Kwahiyo hiyo labda ni kwaajili ya kujua au kuamini? Mi nauliza kwasababu ningependa kujua.” “Well....ahhhh mi sijui bwana.Labda naamini labda siamini.Alafu nasikia njaa , hivi sasa hivi saa ngapi?” niliweza kuona usoni kwake kwamba majibu niliyokua nikimpa sio aliyokua akiyataka maana alitikisa kichwa chake kwa masikitiko kama mtu aliyekua amekosa kile alichotegemea baada ya kusubiri kwa muda mrefu ila sikujali kwa wakati ule.
Yani we Zawadi bwana!Anyway nadhani itakua inakaribia kwenye saa nne hivi. Ngoja nikuangalizie kitu hapo nje, hopefully nikirudi wazee nao watakua wamemalizana na doctor tujue kinachokusumbua.” baada ya kusema hivyo alitoka mara moja bila hata kuuliza ningependelea kula nini.

Nilitumia muda ule niliobaki mwenyewe kufikiria kuhusu mitihani yetu ya mwisho, nitakachofanya iwapo sitofaulu na kazi ambayo ningependa kufanya mbeleni iwapo malengo yangu yangefanikiwa. Sheria, ndicho nilichotaka kusomea hapo baadae. Japo mwanzoni nilitamani na kupenda sana nije kuwa mwalimu hapo baadae nilibadili mawazo pale Rehema,mmoja wa marafiki zangu aliyekosa nafasi ya kujiunga na shule ya sekondari kutokana na kutofanya vizuri sana katika mitihani ya darasa la saba aliposhindwa kuendelea na masomo mwaka uliofuata. Mwanzoni alikua na matumaini ya kuweza kuendelea katika shule binafsi ila matumaini yake hayo yalikatika pale baba yake alipopata ajali ya gari iliyouathiri uti wake wa mgongo, alifariki siku tatu baadae. Pamoja na kwamba familia yake ilikua na hali nzuri mambo yalibadilika pale familia ya baba yake ilipojimilikisha mali zao bila kuwajali. Ghafla walijikuta wanaishi kwenye nyumba ya kupanga japo baba yao alikua amejenga , na duka lao la vifaa vya umeme likakabidhiwa kwa wawili wa baba zake wakubwa bila wao kuhusishwa. Maisha yao yote yalibadilika na sio kwa uzuri ila mama yao hakujua aende wapi ,hivyo akaamua kutumia muda wake kuwatafutia wanawe kitu cha kula badala ya kupambana na ndugu toka upande wa marehemu mumewe. Kwa wakati ule ndo alikua kidato cha tatu maana aliamua kurudia darasa la saba na kufanya vizuri ila bado kile kilichoikuta familia yake kiliusumbua moyo wangu. Mara kwa mara tulipokutana tuliongelea malengo yetu ya baadae na tuliahidiana kujitahidi kadiri ya uwezo wetu kujitengenezea maisha yenye hali ya kuridhisha na kuhakikisha kwamba hatutapata shida kama wapatazo wazazi wetu. Kwasababu yeye alipenda sana masomo ya sayansi yeye alipanga kusomea udakitari na mimi sheria. Nilipanga kwamba nikifanikiwa kusoma sheria ningependa kuwa mtetezi wa kina mama na watoto kuhakikisha kwamba hawanyang'anywi kile ambacho ni haki yao pia kuwahamasisha kuhusu kujituma ili wapunguze nafasi ya wao kunyanyasika kwa kua wategemezi.

Wakati naanza kuvuta taswira ya ambavyo ningependa maisha yangu yawe huko mbeleni nilishtushwa na kelele zilizosikika karibu na chumba changu. Ilikua kama watu wanapigana ama wanapingana kuhusu kitu fulani, nikafikiria kwenda kuchungulia kilichokua kinaendelea ila mpango wangu huo ukaahirishwa na mlango wa chumba nilichokuwamo kufunguliwa bila ya taarifa. Baba aliingia akifuatiwa na vijana wawili pamoja na mzee mmoja ,wawili kati yao walivalia sare za rangi ya kijani iliyofifia na mmoja alivaa kiraia zaidi. Wote wakiwa katika hali ya kushangaza, baba alionyesha kua mwenye hasira na wale wengine walionyesha wasiwasi. Uso wa baba ulikua umekunjamana kwa hasira iliyoonekana hata machoni mwake, shati lake lilikua limekaa upande na hakua na kofia yake kichwani wala mkononi. Sikua na shaka kwamba kelele nilizozisikia mwanzo zilitokana na jopo hilo.Sikupata hata muda wa kufikiria wala kuuliza kilichokua kikiendelea maana baba alifoka kwa hasira huku akielekea pale nilipokua nimekaa huku macho yakiwa yamenitoka kwa mshangao na hofu, “Mpumbavu mkubwa wewe!” alitoa maneno hayo sambamba na kofi la nguvu lililopasha moto shavu langu.
Sikujua hasira yake na maneno hayo yalitokana na nini hivyo sikujua hata mnyenyuko wangu ulitakiwa uwe wa aina gani. Maumivu ya shavu yalinifanya nitamani kudondosha machozi na maneno yake yalinifanya nitamani kuuliza kulikoni ila sikufanya chochote kati ya hayo. Niliishia kukaa kimya huku nikisubiria mkono wake uliokua hewani unifikie tena huku yakwangu ikiwa imefunika mashavu yangu. Kwa bahati nzuri kwangu wale waliongia pamoja naye walimuwahi na kumvuta nyuma kitendo ambacho kilipelekea shati la baba lichanike kidogo upande wa kulia.Kitendo kile kilimwongezea hasira maana alianza kupumua kwa nguvu huku macho yakimtoka kana kwamba alikua tayari kuua mtu. Katika hali ambayo haikutarajiwa nami au wale waliokua wamemshika baba alitumia kiwiko chake cha mkono kumpiga mmoja wao mbavuni huku akiwaambia wamwachie kabla hajawaumiza wote. Pamoja na kwamba kijana aliyepigwa alionekana kuguswa na maumivu kisawasawa bado hakumuachia baba, pamoja walijitahidi kumdhibiti na kumhamasisha apunguze hasira. 

15 comments:

  1. Mamkwe daaah hadithi yaendelea kuwa tamu hongera sana je una mpango wa kutoa kitabu hapo baadae?

    ReplyDelete
  2. Asante mkwe...nafurahi kusikia bado utamu upo upo!!

    Hehheh kuhusu kitabu...labda mkwe!!Tutaona huko mbeleni!

    ReplyDelete
  3. Such a nice story...,Such a nice story...,

    ReplyDelete
  4. Ingekuwa ni movie, basi genre yake ingekuwa ni ''suspense''.

    ReplyDelete
  5. wherever u go... nitaifuata ZAWADI yangu. lizzy lemme say thank u once again...wherever u go... nitaifuata ZAWADI yangu. lizzy lemme say thank u once again...

    ReplyDelete
  6. hadithi ni tamu hongera kwa utunzi mzuri, ila rangi nyeusi na haya maandishi meupe inaumiza macho mno, kama utaweza badili rangi ingekuwa poa sana, siku njema

    ReplyDelete
  7. Mungu azidi kukupa mafunuo zaidi ili kupiia vionjo kama hivi yumkini jamii ipate kuelimika......... yaani ni utamu tupu.

    ReplyDelete
  8. Hongera sana Lizzy! Yani it touches! Huuh! Kitabu lini mamii? God bless u dear..

    ReplyDelete
  9. Mamy uko wapi mbona muda mrefu tunatamani kujua mwisho wake. Hadith kwa hakika ni nzuri sana nigependa niendelee nayo.

    Regards,

    All the best.

    ReplyDelete
  10. Thank you gusy!!
    Mnanipa nguvu ya kuendelea kuandika!!

    Anon pole kwa kuumizwa macho...ntarekebisha soon!!!

    ReplyDelete
  11. WE ARE STILL AT CROSSROAD WHAT WENT ON AFTER THAT

    ReplyDelete
  12. Anon soma sehemu ya saba....

    ReplyDelete