Thursday, August 25, 2011

Zawadi seh. ya pili....

Sehemu ya pili...

Masomo yaliyokua yanafuata baada ya mapumziko yalikua hesabu na fizikia na yote aliyafundisha mwalimu Samea!Nikautumia ukaribu wetu kupata ruhusa ya kuondoka na kuenda nyumbani bila maswali kabla hata somo halijaanza maana nilishaanza kujisikia vibaya.Siku zote nimekua nikiwa na kiwewe au shauku ya kitu fulani napatwa na hali ya ajabu!Kama ni kitu kibaya basi wakati mwingine hua hata tumbo linaanza kuvuruga mpaka kufikia kuniuma,napatwa na hofu mpaka mwili unanitetemeka.Hiyo ndio hali niliyokua nayo na nilijua fika kubaki pale shuleni kusingenisaidia hivyo nikaona bora niwahi nyumbani nijaribu hata kulala kidogo.Na hivi mama alikua hana kawaida ya kurudi nyumbani kabla ya saa kumi na moja sikua na wasiwasi wa maswali ya kwanini nimerudi mapema.

Nilitembea mwendo wa taratibu kuelekea kituo cha daladala cha pale Vijibweni,muda wote huo nilijaribu kujizuia nisiwaze chochote kile hivyo nikaokota kijiti na kuchora mstari mchangani kadiri nilivyokua natembea.

Bzzz bzzzz nilihisi mgurumo ukitokea ndani ya mfuko wa sketi ya kijani niliyokua nimevaa.Niliingiza mkono kivivu mfukoni na kutoa simu niliyonunuliwa na mwalimu Samea miezi nane au tisa iliyopita.“We vipi bwana unaondoka hata huagi?!Usije ukakuta una mimba kweli alafu husemi.Shaurilo!!“ Ulikua ni ujumbe wa simu toka kwa Ester.Bila shaka aliyeandika alikua Mwajei maana yeye ndiye aliyekua mtaalamu wa madongo. Nilifikiria kujibu ila sikua na uhakika jibu gani niwape.Nikaamua niwapotezee mpaka ntakapojua kwa hakika mama alitaka kuongea nini nami ili niwape habari kamili.Kabla sijarudisha simu mfukoni nikakumbuka simu iliyoingia asubuhi.Nikabonyeza vitufe kuangalia simu zilizoingia na kutoka ili kujua aliyenipigia alikua nani maana asubuhi sikuhangaika nayo.Nilikutana na namba ambayo sikua nimeihifadhi mle kwahiyo haikua na jina. “Oya...angalia basi unapoenda.“ ilikua ni sauti ya gadhabu kidogo kutoka kwa mwendesha mkokoteni wa maji ambae kidogo tu nilikua niuvae mkokoteni wake kwa kutoangalia mbele.Nikamwangalia na kumwambia “samahani “ ya kizushi maana sikujali.


Nikachangamsha miguu kumalizia hatua chache zilizobaki kufika kituoni.Bahati nzuri sikua na haja ya kusubiria maana nilikuta tayari kuna daladala mbili zilizokuwa zinasubiria abiria ili waelekee Ferry.Nilichagua ile ambayo ilikua bado sana kujaa sababu sikua na haraka na nilikua natamani kukaa kwa utulivu. “Denti bila sh. 50 haupandi“ yalikua maneno ya konda aliyechafuka vumbi na kunuka jasho!Nikatoa noti ya sh.500 na kumkabidhi “kata ya mtu mzima..nakaa.“ “Alafu nyie madenti siwamaind kabisa.Wote mngetakiwa muwe mnalipa naulia kama watu wazima badala ya kujaza gari bure...au kama vipi serikali iwanunulie za kwenu.“ Alisema huku akinirudishia chenji yangu.Ingekua siku nyingine ningeanza kubishana nae kuhusiana na swala la wao kunyanyasa wanafunzi mpaka kupata mashabiki kati ya abiria wengine ila kwa muda ule sikua na hamu ya kufanya vile.Nikaingia kwenye gari na kukaa siti ya pili kutoka mwisho upande wa dirishani.

MIEZI KADHAA BAADAE!
“Wiki ijayo ndio mitihani inaanza.Maandalizi mliyopata pamoja na juhudi zenu ndivyo vitakavyoamua kama mtatoa maua au miiba.Naomba tusiabishane tafadhali. Mkiniangusha ntawafuata huko huko majumbani kwenu niwalambe bakora, kwahiyo msidhani kwamba ndio tumemalizana. Nawatakia kila la kheri, mjitahidi, mjitume kuonyesha kwamba miaka minne mliyokua hapa mlikua mnasoma na sio kucheza. Kupumzika weekend hii ni muhimu kwa hiyo mambo ya disco subirini mpaka mrudi mtaani. Tutaonana jumatatu.“ maneno haya yalitolewa mwalimu mkuu wa shule, Mrs Matole.Baada ya kumaliza kututisha alianza kuchezea fimbo yake kwa mikono yote miwili huku akitoka nje ya darasa tulilokuwamo.Watu walianza kuongea japo bado kuliwapo na mwalimu aliyebaki pale.Hakufurahishwa na kitendo kile hivyo alichukua rula iliyokuwepo kwenye dawati kwa kwanza kulia na kuligonga dawati hilo hilo mara tatu.Wote tulitulia na kujiweka sawa.Hakua na mengi ya kusema hivyo alifanya kurudia machache tuliyosikia toka kwa mwalimu mkuu akaongezea na kwamba kila mmoja aje akiwa amejiandaa kikamilifu hiyo jumatatu.Kwamba tusije na kalamu zilizoisha wino tukitegemea kupuliziana kwenye chumba cha mtihani.Tuliitikia wote kwa pamoja kuashiria tumemuelewa nae alinyanyua rula aliyokua ameshika na kutupa ishara ya kuondoka.

Watu walianza kutoka kwa fujo kama wafungwa walioachiliwa huru huku wakipiga kelele za shangwe.Nilihisi kuboreka na hali ile maana walikua wananiongezea maumivu niliyokua nayo kichwani tayari.Siku ya nne hiyo tangu nianze kupata maumivu ya kichwa na uchovu usio na mpangilio bila kujua tatizo langu ni nini.Mama alihisi nna malaria ila hakua na pesa ya kwenda kupima hivyo aliniomba nivumilie mpaka jumamosi atakapokusanya baadhi ya madeni anayowadai wateja wake. “Zawa uko poa?!“ aliniuliza Ester huku akichuchumaa ili aweze kuona uso wangu niliokua nimeuinamisha chini. “Yeahh, kichwa tu kinagonga kwa mbali.Tangulieni nakuja.“ nilijibu bila kutazama juu.Mwajei alimvuta mkono akamnong‘oneza kitu kilichowafanya waangue kicheko huku wakitoka nje ya darasa.

Baada ya sekunde kadhaa niliinua kichwa na kugundua kwamba mwalimu Samea hakua ametoka mle darasani na wala hakua amesimama tena...alikua amekaa juu ya dawati macho ameyaelekeza mlangoni.Alipoona hamna mtu mwingine karibu alizungumza kwa sauti ndogo yenye chembechembe za hasira, “Jana ilikuaje hukuja??!“ Nilivuta pumzi ndefu na kuishusha taratibu kabla ya kumjibu kwamba mama alinihitaji nyumbani mapema. “Kwahiyo na simu yano ukazima kwasababu!?“ aliuliza bila kunitazama. “Chaji iliniishia.“ nilijibu kwa ufupi.Nilikua nadanganya nae alijua.

“Tangulia ntakukuta.“ alisema huku akinitupia funguo za nyumbani kwake kisha akatoka na kuelekea ofisini. Sikutamani kwenda ila sio kama alikua ameniomba ama ameuliza kama ntapenda bali aliniagiza hivyo nilipaswa kutii na kufuata maagizo.

Kagiza nilikokakuta ndani kaliyafurahisha macho yangu hivyo niliyaacha mapazia yake nilivyoyakuta na kuelekea moja kwa moja kwenye sofa la watu wawili lililokuwamo mle ndani. Nilijiegesha kwenye sofa huku nikiwaza ntamkimbia vipi mwl pindi atakapofika pale. Nilikua nimeanza kumchukia na ndio sababu haswa ya mimi kumkwepa kila alipotaka kukutana nami faragha. Nilitamani nisingekua na ulazima wa kuonana nae kila siku ila sikua na ujanja, hata hivyo nilipiga moyo konde maana muda sio mrefu nisingekua mwanafunzi tena pale.

Kila nilipokumbuka kile kilichotokea wiki karibu tano zilizopita nilitamani kulia, wakati mwingine kumpiga hata kibao au kumuaibisha mbele ya wanafunzi na walimu wengine. Kama kawaida nilipita kwake baada ya shule na kufanya yale niliyozea huku yeye akiwa bize anatazama TV na mara chache kunitazama mimi niliyekua napika upande wa pili wa sebule. Hakuacha kunitupia sifa za hapa na pale kuhusiana na mke wa aina gani ntakua kwake hapo baadae, siku zote maneno yake yalikua yakinipa tabasamu toka moyoni. Nilikua na matumaini na nilijua nimependwa. Pamoja na kufuatiliwa na vijana wengi wa umri wangu bado niliamini kwamba mwalimu ndio saizi yangu. Simu yangu ilipoita aliitoa kwenye mkoba uliokua pembeni ya sofa alilokalia na kunijulisha kwamba kuna mtu ananipigia. Alikua Jerry, nilipokea na kumsalimu ''Mambo?'' ''Sio shwari wala nini. Ulivyofanya juzi sio fresh kabisak, yani mi niliacha mishe zangu nikakusubiria home pale alafu hukutokea.'' alijibu akionyesha kukereka. '' Tulikua tuko bize tunasoma bwana, muulize hata Ester anajua.'' Nilimjibu kabla ya kumuomba nimtafute baadae maana nlikua na kazi.
''Nani huyo?'' aliniuliza mwalimu. ''Kaka yake Ester.'' ''Alikua anataka nini?'' aliniongezea swali. ''Umm basi tu ananisumbua sumbua.'' nilijibu huku nikipiga hatua kuelekea lilipokuwepo jiko. Bila kutarajia aliomba nimpe simu yangu nami bila wasiwasi nilimpatia.

Kwa zaidi ya dakika kumi hakusema neno wala hakuelekeza macho yake ilipo TV , alikua akihangaika na simu yangu. Mpaka namaliza kupika na kutenga chakula hakuwa anaongea nami, nadhani hata kuniona hakuniona wakati naweka chakula mezani maana nilipomwita alishtuka. ''Chakula tayari hivyo.'' nilimwambia kwa kujiamini. ''Unaweza kuniambia huyu Jerry mmeanzana lini?Maana naona mnatumiana tu maujumbe.'' alisema huku akielekea mlangoni. Kabla sijamjibu nilishangaa kuona anafunga mlango kwa ndani mchana wote ule, kisha akaja nilipokua nimesimama na bilauri la maji mkononi. Akalichukua na kuliweka mezani kisha akasogea karibu sana na nilipokua kiasi kwamba hewa yote niliyovuta ilikua na harufu yake. ''We hunijui ehh?'' ndio maneno niliyoyasikia sambamba na kibao kikali cha shavu. Akili yangu haikuweza kufanya kazi kwa haraka sababu nilishtushwa sana na kile kitendo, nikabaki nimezubaa nisijue cha kufanya.


Itaendelea...

Be blessed...and stay blessed.
L.I.S

1 comment:

  1. what a freak! simpendi huyo mwalimu wako tayari,uwiii! hadithi tamu,nitawapa wanangu!

    ReplyDelete