Wednesday, August 24, 2011

Zawadi......

(Kisa hiki ni cha kutunga, mfanano wowote na watu au matukio halisi ni bahati tu na siyo kusudio langu. Haki zote za kunakili, kuchapa, au kutoa kwa namna yoyote ile iwe ya uchapishaji, digital au vinginevyo zimehifadhiwa. Kisa kizima au sehemu yake hairuhusiwi kutolewa mahali pengine bila ruhusa yangu )




Sehemu ya kwanza...

Alfajiri na mapema nilimsikia mama akiniita kwa sauti niamke.Taratibu nikajigeuza kutoka upande niliokua nimejilaza na kutazama juu kwenye paa letu lililokosa silingi bodi.Bati lililoezeka nyumba yetu ya kupanga lilikua limechakaa kiasi chake ila bado lilikua linatuhifadhi bila kero za kuvujiwa wakati wa mvua japo wakati wa joto dawa yake tuliipata!

“Hivi we Zawadi hunisikii?“ nilishtushwa na sauti ya mama aliyekua ametoka uani kote kuja kunipigia kelele niachane na kitanda. “Mama nawe bwana...nimekusikia sana sema nilikua nasali kwanza ndo niamke.Kwani saivi saa ngapi?!“ “We achana na mambo ya saa.Leo zamu yetu kufanya usafi embu wahi chooni huko kabla watu hawajaanza kupishana upate kisingizio cha kuchelewa shule.Alafu baadae jioni nikumbushe nna maongezi na wewe.“ Wakati ananiagiza yote hayo alikua anaokota nguo nilizotupa chini jana yake na kuniwekea usoni kusudi niziweke sandukuni au kwenye box .Japo hua nakereka sana akifanya hivyo leo sikua hata na pumzi ya kuanza kulalamika..kwanza nlikua nafikiria hicho choo cha jamii kitakua kwenye hali gani asubuhi yote ile na nlivyo na kinyaa ..arrrrrg sijui kwanini tusingekua kila nyumba na choo chao!Mijitu mingine michafu...unakuta biashara zao zimesambaa pembeni sijui hua hawaoni au inakuwaje.Alafu bila hata aibu inaacha hivyo hivyo bila hata kumwaga maji juu juu.

Kabla ya kuinuka kitandani nikakumbuka kauli ya mama...eti ana maongezi na mie.Tangu lini tukataarifiana habari ya maongezi..kama kunigombeza si angenigombeza tu mara moja yaishe?!Sikuwahi kusikia hiyo kauli toka kwake kabla kwahiyo nilibaki nikijiuliza hayo maongezi maongezi gani!Kheee usikute kanishtukia!!Brrr brrrrr mngurumo wa nokia yangu uliotokea chini ya godoro ndio uliyonitoa kwenye mawazo yaliyokua yanataka kunikamata asubuhi asubuhi !Nikainama kidogo pembeni ya kitanda na kuingiza mkono chini ya godoro ili niwahi kujua nani huyo anaetaka kuniletea balaa asubuhi yote hii.Utadhani watu wote sijawaambia wasiwe wananipigia hovyo!Ile naangalia namba nayo ikakata..wala sikutaka kujishukulisha nayo nikainuka kitandani kanga kifuani nikatoka mpaka uani.Baadhi ya majirani tayari walikua wameshateka maji mapema kuepuka foleni na wengine hata vyombo walishaosha.Nikawasalimia kila mmoja kwa namna yake huku nikifuata ndoo ya maji ya chooni ili nikafanye usafi. Baada ya kuchukua maji nikatumia dakika zaidi ya mbili nikitafuta sabuni ya Omo kabla ya kumuuliza mama, “Mama!MAMAA!!!Eti sabuni iko wapi?!“ niliita na kuuliza kwa sauti kubwa japo sikuhitaji kufanya hivyo. “Kama sabuni ya unga babako alimalizia jana.Nenda hapo kibandani kachukue paketi moja ila pesa mpaka baadae...mwambie Swedi ntampitishia jioni.“ Mama alijibu kwa sauti ya uchovu..yani wakati wowote ule ukitaka kumwona akinyong‘onyea omba pesa ya chochote kile.Wakati mwingine nilikua natamani nimsaidie ila ningeanzia wapi..maana ingebidi nijieleze pesa yenyewe nimepata wapi!Kuchezea fimbo na ukubwa wote huu kwakweli ingekua soo..eti mtaa mzima ushuhudie dada mzima nalambwa za ******!Akhaaa!!Hata hivyo nlikua siombi pesa ya nauli au lunch kwahiyo mzigo kidogo niliwapunguzia.

Nilikatisha mawazo yangu hayo na kutoa tabasamu langu wakati napiga hatua nne za mwisho kuelekea kibandani.Swedi aliponiona tu alianza kunikenyulia mimeno yake. “Mambo Zawa mtoto laini kama nyama ya ulimi?!“ alinisalimia kwa mbwembwe.Bila hiyana nami nikamjibu huku nikipepesa macho kuona kama maandazi yalishaletwa, “Hehehe poa tu.Leo nimekua mlaini ehh?!“ “Sasa we unajiona mgumu?!“ Alinijibu kwa swali huku akinyoosha mkono wake kwa nia ya kunishika bega.Nikakumbuka kwamba nilikua nimevaa kanga moja tu na kurudi nyuma kidogo! “Embu acha zako wewe...nipe omo niwahi zangu mie.Alafu pesa baadae...mama kasema ataleta mwenyewe.“ Akanipatia pakiti moja ya omo na kipande cha andazi bila hata ya kumuomba.Nikamuaga na kuondoka...niligeuka nyuma mara mbili baada ya kuhisi ananiangalia na kukuta kweli macho yote kaelekeza kwangu.Hata mteja mpya aliyekua pale ni kama alikua hamuoni.

Baada ya kusafisha choo na bafu nilijimwagia maji mara moja na kujiandaa kwenda shule.Mama nae alikua anajiandaa kwenda kwenye biashara zake wakati baba alishadamka na kuondoka mapema sana kuwahi samaki wakubwa feri.Mimi ndio kwanza nilikua nimeingia kidato cha nne Vijibweni Sec na baada ya miaka mitatu ya kukutana na watoto pamoja na walimu wale wale kila siku nilikua naona kama hamu ya kwenda shule inapungua.Sijui kwasababu nilikua natamani kutokua mwanafunzi tena niishi nipendavyo?!Hivyo ndivyo nilivyokua nimeaminishwa na mwalimu wangu wa hesabu Mr Samea au Supa kama alivyojulikana kwa wengi. Siku moja tulipokutana nyumbani kwake baada ya shule aliniambia kwamba ni vile tu mimi ni mwanafunzi, ningekua sisomi angeshanioa ili tuwe pamoja kwa uhuru.Huwezi amini nilifurahishwa na maneno hayo kwa kiasi gani.Niliamini kwamba hatua hiyo ingebadili maisha yangu..nisingekua mtoto tena bali mtu mzima mwenye maamuzi yake.

Juma nne hiyo hakukua na jipya lolote shuleni zaidi ya masomo tu na umbea.Hata kuongea na Mr Samea nje ya darasa sikuthubutu maana mawazo yangu yote yalikua kwenye maongezi yaliyokua yakinisubiria.Hata mashosti zangu Ester na Mwajei sikuongea nao sana kama kawaida yetu mpaka wakaanza kunikaba na maswali. “Enhe mwenzetu una nini leo sura imekunjika kama mzee?!“ yalikua maneno ya Mwajei hayo.Japo alikua rafiki yangu bado nisingeweza kukataa kwamba alikua binti mmbea sana..na kwakusuta watu ndio usiseme.Yani siku zote nilikua nashukuru kwamba niko nae upande mmoja.Kabla sijamjibu Ester alidakia kiushabiki, “labda ana mimba.“ na wote wakaangua kicheko kabla ya kusogea karibu yangu ili niwape habari motomoto.

“Yani nyie..ndo urafiki gani huo wa kutakiana mambo ya ajabu ajabu hivyo?!Mnataka mzee Fadhili aninyonge ehhh?!“ niliwatupia maswali bila kuwapa walichokitaka.Wakati wote wakijiandaa kusema kitu tulisikia kengele ya kurudi madarasani baada ya mapumziko ya mchana, hivyo na sie tukainuka na kuelekea darasani haraka maana mwalimu wa zamu alikua amesimama karibu kabisa na tulipokaa huku akiwa ameshika fimbo yake mkononi.

Be blessed...and stay blessed.
L.I.S




















No comments:

Post a Comment