Monday, August 29, 2011

Zawadi sehemu ya nne....


Sehemu ya nne.........

Siku iliyofuata tulichelewa kuamka kutokana na uchovu wa hadithi za usiku mzima. Aliyetuamsha alikua Jerry aliyetumwa na mama yake kutukaribisha kifungua kinywa. Aligonga mara mbili kabla ya kufungua mlango na kuingia ndani kwa kunyata, pamoja na kwamba tulimsikia wote tulifumba macho kama vile bado tumelala. Alienda moja kwa moja dirishani na kusogeza pembeni mapazia yaliyokua yakizuia jua lililokua linawaka asubuhi ile lisiingie chumbani . Mwanga wa jua ulimmulika Ester aliyekua amelala karibu na dirisha na kumfanya amfokee Jerry kumwomba arudishe mapazia kama alivyoyakuta. “Amka huko acha uvivu. Alafu we ni muongo kweli, jana siuliniambia Zawadi haji wewe?!“ aliuliza Jerry. “Embu ondoka bwana!Au nimwambie mama unatusumbua...!MAMAA!!“ yalikua majibu ya Ester ambae kwa wakati ule hakua tayari kuamka. “Mama mwenyewe ndio kanituma niwaamshe kwahiyo sitoki wala nini.“ nilishawazoea kwa vile ambavyo walikua wakichokozana mara kwa mara, haikua ajabu sababu umri wao haukuzidiana sana hivyo kila mmoja alitaka kumwonyesha mwenzake kwamba hawezi kumtawala.


Kwakua nilikua nimegeukia ukutani sikua na wasiwasi wa Jerry kuuona uso wangu, ila nilijua iwapo ataendelea kuwepo pale mpaka tuamke atauona tu. Nikavuta shuka tulilokua tumejifunika mpaka kichwani kisha nikatumia mkono wangu kujipapasa usoni ili nione kama bado ulikua umevimba. Nilihisi ulikua umerudi katika hali ya kawaida japo siku na uhakika. Nikageuka na kulala chali kisha nikashusha shuka lile usawa wa ilipoanzia pua yangu kabla ya kumsalimia Jerry , “Mambo msumbufu?!“ “Fresh tu mrembo, umeamkaje?!“ alinijibu kwa uchangamfu. “ Mmmh nimeamka kwa ubavu.Unaweza kutoka kidogo tuvae?!“ sijui kipi kati ya jibu na swali langu vilimfanya atabasamu ila alitabasamu kisha akatoka nje. Mwanzoni mimi na Jerry hatukuwahi kuzoeana sana, tulionana kila nilipokuja kumuona Ester ila hatukuwahi kukaa chini na kuongea , japo alipenda kunitania mara kwa mara , mara nyingi tuliishia kujuliana hali tu basi. Nakumbuka tulianza kuzoeana alipoanza kunitafuta kwenye simu. Mwanzoni sikufahamu ni nani aliyenipigia hivyo kwa karibu wiki nzima sikujibu simu zake mpaka siku nilipowauliza Mwajei na Ester kama walikua wamempa mtu namba yangu.Wote walikataa ila walipenda kuijua namba yenyewe, “Mbona namba yenyewe kama naijua?!“ alidakia Ester baada kuiona. “Nakuja“ alikimbia ofisini na kutoka na mikoba yetu tuliyokua tumeihifadhi tulipotumwa na mwalimu.Akatoa simu kabla ya kuomba kuona tena zile namba!! “Hahahaha.“ Aliangua kicheko huku akituonyesha alichokua akiona, jina la kaka yake. “Wee!!Hahaha, kumbe mwizi mwenyewe tunamjua.Sasa we alipataje namba yako?!“ aliuliza Mwajei. “Mi ntajuaje, muulize mdogo wake huyo hapo.“ ndilo jibu nililotoa wote tukabaki tunamkodolea Ester macho maana yeye ndie aliyekua mtuhumiwa mkuu kwa wakati ule. Baada ya kufahamu ilikua Jerry tulianza kumtumia meseji wakati ule ule kumchezea. Baadae tulijenga mazoea yaliyosababishwa na kuzungumza sana kwa simu pia ana kwa ana.

“Ahhhhh nimechoka!Mi natamani kuendelea kulala.“ alisema Ester huku akijikunyata na kuvuta shuka kivivu. “ We endelea tu, mi naamka nikaoge nianze kujiandaa kwenda nyumbani.“ nilijibu nikiwa tayari nimetoka kitandani na kuchukua kioo kidogo kilichokuwepo kule chumbani. Uso wangu ulionekana kawaida, sikua na sababu ya kua na wasiwasi ila nilipopiga hatua nilikumbuka yaliyonikuta jana yake.

Nusu saa baadae nilishtushwa na kelele za mlango kutoka kwenye kausingizi kalikokatisha kumbukumbu yangu. Kichwa bado kilikua kikiniuma na uchovu niliohisi mwanzo ulikua umezidi maradufu. Mwalimu aliinua pazia moja na kuruhusu jua la jioni ile lipendezeshe muonekano wa kule ndani. Alienda mpaka kabatini na lilipokuwapo bilauri la maji ya kunywa na kumimina katika glass, akanywa kisha akaijaza tena na kuja nayo nilipokua nimekaa akayaweka upande wangu wa meza. “Tunaweza kuongea kidogo Zawadi?!“ aliuliza kwa sauti ya upole nami nikamjibu kwa ufupi “Nakusikiliza.“
“Alright! Zawadi kusema ukweli nimegundua kwamba umebadilika sana wiki hiz za karibunii, umenyong‘onyea mwenyewe hata kutabasamu hutabasamu kama nilivyozoea.Najua mimi ndiye niliyesababisha ila nilitegemea utakua umenielewa mpaka sasa maana nilishakueleza nini kilichonipata siku ile na samahani nimekuomba si chini ya mara ishirini.Naomba unisamehe tafadhali.“ Nilimtazama juu mpaka chini, alivyokua amekaa kinyonge, uso na macho yake yalivyokua yamekaa kipole nilitamani kumwambia nimekusamehe na kumaanisha ila nilipokumbuka alichonifanyia wiki kadhaa zilizopita nilimwona mtu mwingine tofauti kabisa na aliyekaa pale.Hivi anadhani yeye ni nani hata aweze kuniumiza kiasi kile alafu ategemee ntamsamehe tu sababu ameomba?!Eti alitarajia ningekua nimemwelewa, kwanini yeye asijaribu kunielewa mimi ili aache kunisukuma nimsamehe wakati anapotaka yeye mpaka pale ntakapokua tayari?!Nilihisi damu ikinichemka kwa hasira, hakua na shukurani hata chembe.Hivi ni kwamba amesahau ni kwa kiasi gani ningeweza kumtia matatizoni kama ningewaeleza nyumbani?! Nilitamani kuyasema yote hayo kwa sauti ila sikua katika hali ya kujibizana. “Nataka kwenda nyumbani tutaongea siku nyingine.“ ndio jibu pekee alilopata toka kwangu. “Zawadi please.Yani hujui tu ni kiasi gani naumia kukuona ukiwa hivi, kama ningeweza kurudi nyuma haki ya Mungu nakwambia ungekua unacheka kwa furaha sasa hivi.“ nilihisi kwamba alimaanisha alichokua akikisema.Ghafla nilihisi kizunguzungu ila kabla sijapata nafasi ya kumwambia najiskia vibaya nilipoteza fahamu.


Nilishtuka baadae kwa kuhisi mwanga mkali machoni, nilipojaribu kuinua mkono wangu wa kushoto ili niutumie kukinga mwanga ule nipata maumivu kidogo nyuma kiganja. “Aaaaahhh!!“ niliguna kwa sauti.
“Unajisikiaje?!“ iliniuliza sauti ya kike. “Nimechoka alafu kichwa kinaniuma.Niko wapi?!“ niliuliza huku nikifungua macho taratibu ili kujua nilipo. “ Usijali uko hospitali, embu naomba uniambie unaona nini?!“ nakuona wewe...nilitaka kujibu ila sikufanya hivyo! “Vidole!Viwili!“ nilisema na kuanza kupepesa macho kule ndani. Aliyekua akiniangalia alikua dada mrembo kweli.Alikua amevalia kagauni keusi kalikofika chini tu kidogo ya magoti yake na koti jeupu lililokaribia urefu wa kagauni kake kalikoushika mwili wake wa saizi ya kati vizuri.Alikua mrefu kiasi hivyo viatu vya chini alivyokua amevalia vilimkaa vyema pamoja na gauni lake. Mkononi alishika kalamu na file alilokua akiandika alichojua yeye. Nywele zake zilikua zimenyolewa karibu kuisha, kama asingekua mzuri wa asili ingekua rahisi kumfananisha na mwanaume.Macho yake yalikua ya mviringo na makubwa kiasi huku yakisindikizwa na pua pana kidogo iliyoendana na uso wake.Kama asingekua daktari hakika kujishughulisha na maswala ya urembo kungemfaa mno.


Hakukua na mtu mwingine mle ndani zaidi yangu na yeye, hata kitanda kilichokuwepo upande wa pili kilikua kitupu.Katikati kulikua na meza iliyotenganisha vitanda vile viwili na juu ya meza kulikua na maua mchanganyiko. Pembeni ya kitanda changu ilisimama chuma kubwa maalumu kwa kuwekea dripu.Juu yake ulining‘ininzwa mfuko uliokua una maji, au sijui ilikia dawa iliyokua ikidondoka matone madogo madogo kila sekunde kuelekea mwilini mwangu.

Sikuhitaji kuuliza nilifikaje pale ila nilipenda kujua aliyenileta yuko wapi hivyo nikamuuliza yule daktari.“ Yuko nje hapo alikua anasubiria nikuangalie kwanza.Natoka niongee nae kidogo alafu atakuja kukuona, sawa ehh?!...Alafu, kwani ni nani wako?!“ aliuniuliza huku akinitazama kiupande.Nilijibu haraka bila kufikiria “Ndugu.“ “Ok!Ntarudi tena baadae kidogo“ aliaga na kutoka huku akirudishia mlango nyuma yake.Kutokana na koti kubwa alilokua amevaa sikuweza kuona umbo lake lilivyokua kwa nyuma ila bado ilibaki mawazoni mwangu kwamba alikua dada mrembo kama sio mzuri.
Nilikumbuka mazingira yaliyonifanya nipoteze fahamu ila sikuwa najua ni kwa muda gani nilibaki vile.Nilipapasa macho kwenye kuta zote za chumba kile kuona kama kunasaa ila niliambulia patupu.Sikua na ujanja bali kusubiri huku nikihesabu matone ya dripu yalivyokua yakidondoka.Muda sio mrefu aliingia mwalimu huku akifunga mlango kwa tahadhari . “Zawadi, unajisikiaje?!“ aliniuliza kwa sauti ya chini. “Hovyo!“ nilimjibu.
“Pole .Ila daktari amesema utakua fresh tu, ndo wanaangalia angalia vipimo wajue tatizo nini.“ sikua na haja ya kujua hayo yote ila haikua mbaya kusikia sauti yake.Nilijisikia vibaya kidogo maana nilijua atakua alishtuka sana nilipopoteza fahamu, ndipo nikakumbuka kwamba nyumbani walikua hawajui nilipo. “Saa ngapi sasa hivi?!“ nilitaka kujua. “Ummm saa kumi na mb...ahhh moja kasoro.“ “Nataka kumjulisha mama niko wapi asije akapata presha .Naweza kuazima simu yako?!“ nilimuuliza huku tayari nikiwa nimekinga mkono tayari kuipokea. Bila kusema chochote aliitoa mfukoni na kunikabidhi. “Halo!“
“Shkamoo mama Asha!Zawadi hapa!“ nilimsalimu jirani yetu.
“Mara haba mwaya, hujambo?!“
“Mi mzima!Naomba kuongea na mama kama upo karibu na nyumbani ehh?!“
“Tena niko nae hapa!!Haya huyu hapa...!“ alisema na kumkabidhi mama simu.
“Mama!“
“Zawadi naona sasa umefanya mazoe kuzurura utakavyo na kupiga simu utadhani ulipoondoka nyumbani ulishindwa kuaga na kusema kama utapita kwa wenzako.Alafu wewe si juzi tu ulikua huko?!Au ndo umehama nyumbani?!“ alinipokea kwa maswali kede wa kede.
“Mama!Sikiliza bwana, nipo hospitali.Nilianguka shuleni mwalimu akanileta hospitali sasa hivi ndio daktari kaniruhusu kuongea na simu!!“ sijui kwanini nilidanganya ila nadhani ilikua sahihi kwa wakati ule. “Kheeee!We mtoto, sasa unaendeleaje?!Embu nikamtafute baba yako tuje kukuona.Kwani uko hospitali gani?!“ nilihisi mabadiliko kwenye sauti yake hivyo nikajaribu kumtuliza kidogo!! “Sasa hivi najisikia nafuu.Nadhani ni kile kichwa tu na jua vilichangia!“ nilimjibu kisha nikamuuliza mwalimu kwa kunong‘oneza jina la hospitali tuliyokuwapo! “We unaongea na nani hapo?!“ kumbe mama alinisikia nikinong‘ona. “Mwalimu aliyenileta, nlikua namuuliza tulipo.“ nilimjibu. “Embu nipe niongee nae!“ bila swali wala ishara nilinyoosha mkono wangu wenye simu kuuelekeza alipokua amesimama mwalimu akiniangalia! “Mama anataka kuongea na wewe....“ nilisema huku nikijiuma midomo yangu ya chini.Alipokea simu toka mikononi mwangu na kutoka nayo nje ya chumba tulichokuwemo.

No comments:

Post a Comment